Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa wafanyikazi wa vyuo vikuu KUSU unanuia kuandaa mgomo hivi karibuni kushinikiza nyongeza ya mishahara.

Akizungumza katika kongamano lililoleta pamoja miungano ya KNUT, UASU na TUC-Ke siku ya Ijumaa jijini Mombasa, mwenyekiti wa muungano wa UASU profesa Sammy Kubasu alisema kuwa mgomo mkubwa unatarajiwa hivi karibuni kushinikiza nyongeza ya mishara yao.

Kubasu aliilaumu serikali kwa kukiuka agizo la mahakama la kuwalipa walimu wa shule za uplili na msingi nyongeza yao ya mishahara kama ilivyohitajika.

Aidha, aliongeza kuwa ni lazima miungano ya wafanyakazi kushirikiana kwa kuwa matatizo yanayowakumba walimu yanaweza kuwakumba wafanyakazi wengine wa umma katika sekta mbalimbali.

Wakati huo huo, mweka hazina wa muungano wa KNUT John Matiangi alisema ili wafanyikazi wa umma kupata haki yao na kuepuka kunyanyaswa, ni lazima tume ya kutathmini mishahara SRC ivunjiliwe mbali.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mwenyekiti wa kitaifa wa muungano wa wafanyikazi TUC-Ke Tom Odege, aliyesema kuwa kuna haja ya miungano hiyo kuungana na kutafuta sahihi kwa wafanyikazi wa umma ili kumuondoa Sara Serem katika wadhifa wake.