Wafanyikazi waliosimamishwa kazi mwezi mmoja baada ya kusemekana waliajiriwa kwa njia isioyokuwa halali waliandamana kulalamikia jinsi walivyosimamishwa kazi.
Wafanyikazi hao walitaka kupokezwa barua kutoka bodi ya kuajiri wafanyikazi katika bunge la Kaunti ya Kisii, kuonyesha kuwa hawataruhusiwa kuendelea kutumikia serikali ya kaunti hiyo.
Wafanyikazi hao waliandamana siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii kuelekea ofisi za Gavana James Ongwae huku wakiimba nyimbo za kukashfu bunge la kaunti hiyo.
Waandamanaji hao walitaka kuelezwa lile lilisababisha kufutwa kwao na kupokezwa barua ambayo itaelezea bayana kufutwa kwao.
Waandamanaji hao wakiongozwa na Peter Ochoke walikashifu serikali ya kaunti hiyo kwa kuwasimamisha kazi kwa kutofuata njia mwafaka.
Akizungumza na waandamanaji hao nje ya jengo la bunge hilo la Kisii, Spika wa bunge hilo Okerosi Ondieki, aliwaomba kutulia kwani kamati ya bunge hilo linaendelea kutafuta suluhu halisi kuhusiana kusimamishwa kwao kazi na kuwapa ripoti au jibu halisi.
“Naomba mtulie kwani kamati ya bunge inaendelea kujadili mahitaji yenu na pindi majadiliano hayo yatakapokamilika, mtapokezwa habari kamili,” alisema Ondieki.
Wafanyikazi hao zaidi ya 100 waliajiriwa Septemba 3, 2014 na hawakulipwa kwa madai kuwa waliajiriwa kwa njia isiyo halali.