Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafuasi wa Muungano wa Jubilee mjini Mombasa wamemkosoa Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar kutokana na hatua yake ya kuikosoa serikali.

Wakiongozwa na kaimu mweka hazina wa chama hicho Salim Bajaber, wafuasi hao walimtaka Seneta Omar kukoma kuikashifu Serikali ya Jubilee wala kumdhalilisha Rais Uhuru Kenyatta.

Katika kikao na wanahabari uliyofanyika nje ya makavazi ya Kitaifa ya Fort Jesus mjini Mombasa siku ya Ijumma, Bajaber alisema kwamba matamshi ya Omar ni yakupotesha wakazi na wakamtaka kushughulikia maswala yanayoisibu Kaunti ya Mombasa.

“Tumechoshwa na matamshi ya seneta wetu wa Mombasa Hassan Omar kuzidi kumkashifu rais wa taifa hili kila uchao. Yeye ni kiongozi na anastahili kuwajibikia Wakenya badala ya kutoa matamshi yasiofaa katika mikutana ya hadhara,” alisema Bajaber.

Bajaber alimtaka Omar ayaangazie maswala muhimu ya vijana na jamii katika kaunti hiyo badala ya kupotoshwa kimaadili na wanasiasa.

Hata hivyo, Seneta huyo wa Kaunti ya Mombasa amewaapuza wafuasi hao na kusema kwamba ana uhuru wa kutekeleza majukumu yake ya kisiasa kama seneta nchini.