Wakulima katika kaunti ya Kisii wanaojihusisha na ukulima wa samaki wametakiwa kujiepusha na kuvua samaki wao wakiwa bado hawajafika kiwango cha umri wa kuvuliwa.
Akiongea siku ya Jumanne katika afisi yake, afisa wa kusimamia kitengo cha mafunzo ya nyanjani na yale ya utaalamu wa kufuga samaki katika idara ya samaki kwenye kaunti ya Kisii Bw Abel Morang’a, alisema kuwa si halali kuwatoa na kuvua samaki wakiwa wachanga.
Aliwashauri wakulima wa samaki walio na vidimbwi katika maboma yao kuhakikisha kuwa samaki wao wanafikisha kiwango cha umri wa kati ya miezi kumi hadi miezi kumi na miwili kabla ya kuwavua.
Alisema kuwa hayo yakizingatiwa, wafugaji samaki watafaidika pakubwa kwani samaki akiwa amefikisha idadi hiyo ya miezi huwa na uzani mkubwa na kwahivyo humfaa mkulima kwa kuwa ataweza kuwauza samaki hoa kwa bei nzuri.
“Wakulima pia wanapaswa kuwa karibu na samaki wao na kuzingatia zile taratibu za kitaalamu za kutunza samaki pamoja na vidimbwi kama vile kuyatoa maji machafu na kuhakikisha maji safi yanaratibishwa kwenye kidimbwi kila mara mkulima anapovuna samaki wake kidimbwini,” alisema Morang’a.
Morang’a alisema wakulima wote walio na azmio la kujiendeleza katika vitengo mbalimbali kushiriki katika mafunzo ya nyanjani yanayotolewa na maafisa wa kilimo katika kaunti hiyo.