Wagema wa pombe haramu ambao wanaendesha biashara yao kisiri katika lokesheni ya Nyamakoroto wameonywa vikali na naibu wa chifu wa eneo hilo.
Tangu kuanzishwa kwa operesheni ya kuharibu pombe haramu nchini majuma kadhaa yaliyopita, viwango vya utumizi vimepungua, lakini wagema wameamua kuuza pombe hiyo kisiri licha ya vikwazo vikali vilivyowekwa.
Wakaazi wa lokesheni ya Nyamakoroto, wakiongea na huyu mwandishi walisema kwamba pombe hiyo imehamishwa manyumbani na kupelekwa katika vichaka inakouziwa sasa.
Naibu wa chifu huyo, Paul Monda aliwaonywa wote wanaojihusisha, wakati alipokuwa akihutubia wakaazi hao wakati wa baraza aliyoiandaa katika uwanja wa shule ya msingi ya Nyamakoroto mnamo siku ya Jumatatu.
“Nataka kuchukua nafasi hii kuonya mgemaji yoyote atakayepatikana akiuza pombe kokote kule, atakabiliana na mkono wa sheria vikali,” alisema Monda.
Vilevile, aliweza kuwaomba wananchi kushirikiana kwa pamoja ili wapige vita pombe haramu, kwani bila wao kutoa habari zozote hakuna atakayejua lolote kuhusu pombe hiyo.
Kampeni hiyo ya kusafisha mitaa kutokana na pombe haramu ilianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta, na imekuwa ikiendelea katika maeneo mengi nchini.