Idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kwa wingi ili kupokea matibabu ya bure yaliyoandaliwa na chama cha Sunni Muslim Anjuman katika msikiti Hidaya, jijini Mombasa.
Mwenyekiti wa chama hicho Haji Musa siku ya Jumapili alisema kuwa hatua hiyo inalenga kusaidia walio na shida za kiafya na wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu.
Kando na matibabu ya macho, wananchi pia wamepokea vipimo vya kisukari pamoja na upashwaji tohara kwa watoto wadogo.
Musa vile vile alitoa changamoto kwa walio na uwezo wa kutoa huduma ya bure kwa wananchi, akisema kufanya hivyo nikusaidia jamii kwani wengi hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
“Lengo letu ni kusaidia wasiojiweza kukidhi matibabu kutokana na hali ngumu ya maisha na tutazidi kufanya hiyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa,” alisema Musa.
Aidha ameongeza kusema huduma zitolewe kwa wananchi wote bila ya kuzingatia dini wala kabila.
Kulingana na mgonjwa Saumu Salim ambaye anashida ya macho alisema amefurahishwa na matibabu hayo na kutoa shukhrani kwa wasimamizi wa matibabu hayo kwa kile alichodai kuwa amepata huduma bora.
“Nafurahi nimepata matibabu ya macho ya bure kwa sababu macho yangu yamenisumbua kwa muda mrefu bila kupata tiba yoyote,” alisema Salim.