Wakongwe kutoka wadi ya Gesima wamepata sababu yakutabasamu baada ya wahisani kutoka Marekani kujitokeza kumaliza ujenzi wa makao ya wazee uliokuwa umeanzishwa na mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba Mwancha Okiemo.
Akiongea katika eneo hilo mwenyekiti wa wahisani hao Bw Daniel Onsomu alisema kuwa wahisani 20 kutoka Marekani tayari wamejitokeza kusaidia kumaliza jengo hilo huku akiongeza kusema kuwa taarifa muhimu kuhusiana na mradi huo zitawekwa wazi baada ya mradi huo kukamilika.
"Tumefanya mazungumzo na mbunge wa zamani Okioma ambaye tayari ameturuhusu kumaliza ujenzi huo, na tunatarajia ujenzi huo kukamilika baada ya miezi saba. Baada ya hapo, tutaweka wazi ripoti kwa umma kuhusiana na mradi huo," alisema Onsomu.
Onsomu aliongeza kwa kusema kuwa jengo hilo linatarajiwa kuweka idadi ya watu kati ya 80 hadi 150 huku akisisitiza kuwa watakao faidi kutokana na mradi huo ni wazee wa zaidi ya miaka 80 na wasio jiweza kiuchumi.
"Nafasi za kwanza zitatengewa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 huku pia tukizingatia hali zao za kiuchumi," alisema Onsomu.
Onsomu aidha aliongeza kwa kusema kuwa kamati maalum itabuniwa ili kuendesha shughuli mbalimbali kwenye makao hayo na hata pia kuajiri wafanyikazi.