Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu wa chifu katika lokesheni ya Nyanguru eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii, Enock Omanwa, amewaomba wahisani wema kujitolea kutoa msaada kwa watu wanaoishi na ulemavu katika lokesheni hiyo.

Wito huo umetolewa baada ya baadhi ya watu wanaoishi na ulemavu katika lokesheni hiyo kusajiliwa ili kupokea msaada wa walemavu lakini kwa bahati mbaya, hawajafanikiwa kupata msaada huo hadi sasa.

Akizungumza siku ya Jumapili katika lokesheni hiyo, Omanwa alisema kuna walemavu ambao wamesumbuka kwa kiasi kikubwa katika lokesheni hiyo ya Nyanguru na wanahitaji msaada ili kuwaokoa.

Kulingana naye, kuna walemavu wawili katika lokesheni yake wenye umri wa zaidi miaka 35 ambao hawana uwezo wa kutembea kamwe na hawana kitimagurudumu wanayoweza kutumia kufuatia hali ya umaskini.

“Kuna wakati walemavu wa kila aina walisajiliwa ili kupata msaada lakini baadhi yao katika lokesheni hii hawakufanikiwa kupata msaada huo. Naomba wahisani waweze kujitolea ili kutoa msaada ili walemavu hawa wanunuliwe kitimagurudumu ili nao weweze kutembea,” alisema Omanwa.