Wahudumu wa magari katika mji wa Keroka, Kaunti ya Nyamira wameiomba serikali ya kaunti hiyo kukamilisha ukarabati wa kituo cha magari katika eneo hilo ili kurahisisha uchukuzi katika eneo hilo.
Wakiongea siku ya Jumatatu na Waandishi wa habari katika mji wa Keroka eneo Bunge la Kitutu Masaba Kaunti ya Nyamira, wahudumu hao wameiomba serikali ya kaunti hiyo kaharakisha kukarabati na kukamilisha kituo hicho ambacho kilianzishwa mapema mwaka huu hadi sasa bado kukamilika.
Aidha, walisema kuwa wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kwani mahali walitengewa kutumia kama kituo, wasafiri wengi hawapajui inayopelekea biashara zao kurudi chini huku wakiiomba serikali kushughulikia jambo hilo kwa haraka.
“Biashara zetu zimerudi chini kwa kuwa wasafiri wengi hawajui kituo hiki kwani walikuwa wamezoea kituo cha zamani. Naiomba serikali yetu ya Kaunti ya Nyamira kutushughulikia ili tuweze kurudi katika kituo hicho na kuendelea na biashara yetu kama kawaida,” alihoji Rodgers Mogeni, mhudumu wa magari.
Kwa mujibu wa wahudumu hao, kituo hicho cha Keroka ina wahudumu wa magari wengi ambao huenda katika sehemu mbali mbali kama Gesusu, Nyansiongo na Gesima ambao walisema wanakosa pahala ya kufanyia shughuli zao.
Wahudumu hao pia walisema kuwa jambo la kuwashangaza ni kuwa kituo hicho ambacho kinachokarabatiwa wafanyibiashara wa mboga wanaruhusiwa kufanyia biashara zao, jambo ambalo limeleta mtafaruko kwao kama ni kituo ama ni soko.
“Serikali ya Kaunti ya Nyamira inastahili kukamilisha ujenzi wa kituo hiki kwa kuwa tumekuwa tukisubiri kwa muda mwingi na hatuoni kinachoendelea,” alihoji Kelvin Mosira, mhudumu wa magari za Gesusu.