Wakaazi wa wadi ya Gesima, eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira wamemwomba mbunge wao kuleta maendeleo badala ya kupiga vita gavana wa kaunti ya Nyamira.
Wakiongea siku ya Jumanne na mwandishi huyu katika eneo la Gesima, walisema kuwa mbunge wao Timothy Bosire anastahili kuwajibika na kufanya maendeleo katika eneo bunge lake la Kitutu Masaba badala ya kusema gavana wa kaunti hiyo hajafanya maendeleo.
Wakazi hao walisema kuwa barabara katika eneo hilo ziko katika hali mbaya na zinastahili kukarabatiwa na serikali kuu kwa ushirikiano na mbunge huyo.
"Barabara ni mbaya na hazipitiki. Mbunge wetu anastahili kuangalia jinsi ya kukarabati barabara hizi na huu sio wakati wa kuandamana ni wakati wa maendeleo," alisema Barongo Mose, mkaazi.
Aidha, wamewomba mbunge huyo kushirikiana na serikali ya kaunti ya Nyamira ili kuinua viwango vya maendeleo kama kaunti zingine.
“Wabunge wote wa kaunti hii wakishirikiana na serikali ya kaunti yetu viwango vya maendeleo vitainuka ili kaunti yetu iwe kama kaunti zingine kimaendeleo,” alisema Boaz Obiria, mkaazi.
Kulingana na wakaazi hao huu si wakati wa maandamano na siasa bali ni wakati wa kuungana ili kuleta maendeleo.
“Tunachotaka ni maendeleo na kama kuna jambo ambalo linastahili kutatuliwa tunaomba viongozi wetu kuwa pamoja ili wawe wanatatua shida na kupata suluhu kwa njia ya amani,”alisema Grace Mokaya, mkaazi.