Mwanasiasa aliyewania kiti cha ubunge eneo bunge la katika Kitutu chache Kaskazini kaunti ya kisii, Atandi James, amewaomba wakaazi wa eneo bunge hilo kutotegemea pesa za wanasiasa ikiwa wanahitaji kuwa watu wa maana na wa kuheshimika siku za usoni.
Akizungumza na wakaazi wa eneo hilo siku ya Jumapili, katika eneo la Masakwe, mwanasiasa huyo hakufurahishwa na jinsi wakaazi walivyokuwa wakimwitisha pesa.
Jambo hilo lilimkera na aliwaomba wakaazi hao kutafuta mbinu mbadala ya kujitafutia riziki ya kila siku na kutotegemea pesa za wanasiasa.
“Sisi wanasiasa tunatembea katika maeneo haya mara moja kwa mwaka au baada ya miaka miwili. Tusiporidi katika maeneo haya mtakuwa munapata pesa kutoka wapi?” aliuliza Atandi.
“Naomba mtafute njia ya kupata riziki ili muonekane kama watu wa maana siku za usoni. Nawaomba muondoe hiyo roho ya kutegemea pesa za wanasiasa kama munataka kujitoa katika hali ya umaskini,” aliongeza Atandi.
Mwanasiasa huyo alionekana kuwalenga sana vijana ambao hawafanyi kazi na wanaotarajia kuvuna mahala wasipopanda.
“Vijana wenzangu, mimi ni kijana kama nyinyi mbona msijiunge kwa makundi ili muweze kujisaidia nyakati zijazo? Kuna pesa serikali imetoa kwa vijana pamoja na akina mama haswa zile za Uwezo Fund. Naomba mtazame mbele na mutumie pesa hizo kabla hazijarudishwa katika hazina ya serikali,” alisisitiza Atandi.