Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wanaotumia kivukio cha feri cha Likoni wamewashinikiza wasimamizi wakuu wa Shirika la Huduma za Feri nchini kutenga sehemu maalum ya watu wanaoishi na ulemavu ili kuepukana na misukumano ambayo hushuhudiwa katika kivukio hicho.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wamiliki na wahudumu wa tuk-tuk katika kaunti ya Mombasa Obedi Muruli, walisema mara nyingi jamii hiyo hupitia changamoto nyingi katika eneo la kivukio hicho na akasema kwamba kuna haja ya kutengwa sehemu maalum ya jamii hiyo.

Katika mahojiano ya moja kwa moja na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Muruli alisema iwapo wasimamizi wa shirika hilo la hudumu za feri nchini hawatazingatia shinikizo hilo, basi walemavu wanaotumia kivuko hiyo watazidi kujeruhiwa, hali ambayo kulingana na Muruli ni ukiukaji wa haki za kibinadamu.

“Tunaomba shirika la huduma za feri kuwatengea walemavu mahali maalum kusubiri wakati wa kuabiri feri ili kuwaepusha na misukumano ambayo hushughudiwa kila wakati wakazi wakiabiri feri hususan wakati wa asubuhi na jioni," alisema Muruli.

Alipendekeza shughuli hiyo kutekelezwa kwa muda wa wiki moja ili kupunguza majeruhi katika kivukio hicho na kuisaidia jamii hiyo kutumia feri hizo kwa upole kwani kulingana na hali yao ya kimaumbile ni changamoto kubwa sana kwao.

“Tumewapa wasimamizi wa shirika hilo kipindi cha wiki moja kuwatengea walemavu na wanawake wajawazito kwani bila ya shughuli hiyo kutekelezwa basi huenda majanga yakatokea," aliongeza Muruli.

Mapendekezo hayo yamejiri siku chache baada ya wakazi kujeruhiwa wakati walipokuwa wakiabiri feri kutokana na msukumamo uliyotokea katika kivukio hicho.