Zaidi ya wakazi 300 kutoka mitaa ya mabanda ya Dunga Unuse na Mbuyuni eneo bunge la Changamwe, wamebomolewa nyumba zao katika zoezi la ubomozi uliokuwa ukitelekezwa kupitia uamuzi wa mahakama uliotolewa mwezi wa pili mwaka huu.
Wakazi hao walidai kuwa ubomozi huo ulikuwa kinyume na sheria huku wakiitaka serikali ijukumike katika mawasiliano na mipangilio bora katika uhamisho.
Aidha, wakazi hao wamewataka wazee wa kaya kuishinikiza serikali kuwapatia makao ili waweze kuishi vyema kwa kutekeleza mila na itikadi zao katika eneo hilo la Dunga Unuse.
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipangilio katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya, ameafikiana na madalali hao wa ubomozi kusimamisha ubomozi huo ili kupata mipaka mwafaka na kuhakikishia kuwa wakazi watapata amani kwa kupata makazi yao.
Thoya aliwalaumu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa na Mwenyekiti wa Tume ya Ardhi Mohammed Swazuri kwa kuendeleza mzozo huo kwa kushinikiza kufurushwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Vile vile, Thoya amewataka wakazi wa eneo la Dunga Unuse kutokubali kugawanywa kwa misingi ya kidini wala kikabila na baadhi ya mabwanyenye wanayoitaka ardhi hiyo iliyoko mita chache kutoka bandari ya Mombasa.
Haya yanajiri baada ya wakazi hao kupata onyo ya kufurushwa katika maeneo hayo wiki iliopita.
Kesi za ardhi zimeendelea kuhangaisha wakazi mbali mbali katika kaunti mbali mbali zikiwemo ya Kwale, Mombasa na Kilifi bila wakazi kupata suluhu kwa mizozo hiyo.