Wakazi wa mtaa wa Changamwe wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kukarabati mabomba ya kupitisha majitaka ambayo yanavuja.
Wakizungumza siku ya Alhamisi Kupitia Suleiman Ahmed, mzee wa mtaa, ambaye pia ni mmiliki wa nyumba katika sehemu hiyo, wakazi hao walisema kuwa mabomba yanayotoa majitaka kutoka ploti hizo pamoja na mashirika ya viwanda vya kuchakata bidhaa mseto katika eneo hilo, yako katika hali mbaya na ni hatari kwa afya za wakazi.
Mzee huyo alisema kuwa maji hayo mara nyingi huweza kuenea hadi mahali pa kufanyia biashara, ikizingatiwa kuwa wengi wa wakazi wa eneo hilo hutegemea biashara ndogo ndogo kama zile za kuuza mboga na vyakula.
Ahmed aliiomba wizara ya afya kutembelea eneo hilo ambalo linaendelea kukua kwa kasi na kuitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kulipa eneo hilo kipaumbele kwenye masuala ya uboreshaji wa majengo pamoja na kuwatengezea masoko ili kuimarisha uchumi wa wakazi.
"Tunaiomba serikali ya kaunti yetu ya Mombasa itutengenezee na kukarabati mabomba pamoja na barabara za kuingia katika mitaa hii ambazo zimeanza kuwa katika hali mbaya," alisema Ahmed.
Alisema kuwa swala hilo linafaa kushughulikiwa kwa haraka ili kuzuia wakazi kuambukizwa maradhi yanayosababishwa na uchafu kama kipundupindu.