Share news tips with us here at Hivisasa

Chifu wa Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu, Sally Letting, amewahakikishia wakazi wa eneo hilo usalama.

Haya yanajiri baada ya kushuhudiwa visa vya uhalifu hivi majuzi.

“Tuko na usalama wa kutosha na ni wajibu wetu kama serikali kuhakikisha kuwa kila moja wenu anapata usalama wa kutosha,” alisema Letting.

Akiwahutubia wakazi katika mbio za amani almarufu kama MUKESCO siku ya Jumamosi, Letting alisisitiza kuwa usalama unaanza na kila mmoja kuhakikisha kuwa anaripoti visa vinayoshukiwa kuwa vya uhalifu kwa polisi.

Chifu huyo vile vile aliwapongeza wanariadha na jamii mbali mbali kwa kujitolea kushiriki katika mbio hizo za amani akisema kuwa ni njia mwafaka ya kukuza jamii na kuishi kwa amani.

“Kupitia riadha, tutaishi kama dada na ndugu. Tunajivunia kama jamii ya Kesses kuwa na makabila yote 42, dhihirisho tosha kuwa tunaishi kwa amani,” alisema Letting.

Mwakilishi wa wadi ya Megun, Peter Sugut, alimunga mkono chifu huyo kwa kusema kuwa amani ni chanzo cha utajiri na huleta upendo kwa wote.

Mbio hizo za amani zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo mwakilishi wa Naibu chansela wa Chuo kikuu cha Moi Profesa Nathan Ogechi, Mwanariadha Lornah Kiplagat, wawakilishi wa kaunti na mwakilishi kutoka shirikisho cha wanariadha miongoni mwa wengine.