Huku baadhi ya sehemu nyingi katika eneo zima la Gusii zikiwa tayari zimeanza kupokea mvua nzito, Wakazi kutoka kaunti ya Kisii wametakiwa kutumia nafasi hiyo kuhifadhi maji ya mvua ya El Nino ili kuyatumia nyakati za kiangazi kunyunyizia mimea yao.
Akiongea katika afisi yake siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu wa idara ya hali ya anga katika kaunti ya Kisii, Henry Sese, alisema kuwa watu hawafai kuona mvua nyingi kama laana bali waitumie kama baraka kwao, kwa kukinga maji hayo na kuyahifadhi.
Alishangaa ni kwa nini wengi wa wakulima hasa kutoka kaunti za Kisii na Nyamira wamekuwa na mtindo wa kuacha maji yakimwagika chini, na nyakati za kiangazi ndio huwa wanakumbuka umuhimu wa maji.
Aliwataka wakazi kuanza kukumbatia kilimo cha kisasa cha kunyunyuzia mimea maji na kukumbuka kuwa eneo la Kisii siku hizi huwa na kiangazi kinyume na siku za awali ambako kulikuwa kunashuhudiwa mvua kila mara.
“Wakazi na wakulima sharti wachukue nafasi hii kuhifadhi maji ya mvua. Hii ni baraka kubwa na watu wetu wanahitaji kuichangamkia. Imekuwa mazoea kwetu hapa eneo la Gusii kupuuza maji ya mvua na kuwa na matumaini kuwa sisi tuna mvua kila mara na kusahau kuwa joto la viwanda ulimwenguni limeathiri uataratibu wa hali ya anga,” alisema Bwana Sese.
Mkurugenzi huyo aliahidi kushughulikia suala la El Nino kwa kushirikiana na idara zingine katika kaunti kwa kuwafaa wakazi kwa jumla.