Wakazi wa Kaunti ya Kisii wamehimizwa kuziba vidibwi vya maji vilivyoko karibu na nyumba zao ili kuzuia umbu na usabazaji wa ugonjwa wa malaria.
Akiongea siku ya Jumapili katika kijiji cha Gekomu, mhudumu wa afya ya Jamii Kepha King’oina alisema kuwa kuna ongezeko wa mbu wa malaria katika eneo hilo kutokana na vidibwi hivyo.
Mhudumu huyo aliwaomba wakazi kuziba vidibwi hivyo kama njia moja ya kuzuia ugonjwa huo.
“Nawaomba wakazi wote wa kaunti ya Kisii kuziba vidibwi hivyo ambavyo havina maana kwa jamii kwani vimechangia kuwa na umbu wengi katika kaunti ya Kisii,” alisema King’oina.
Aidha, alisema kuwa serikali ya kaunti kwa ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kila mkazi atapokezwa neti ili kuzuia vifo vinavyotokana na malaria.
“Serikali ya kaunti kupitia Wizara ya Afya imeweka mikakati ya kuwapa wakazi neti lakini ni wajibu wa kila mkazi kuhakikisha kuwa mazingira ni safi kila wakati, ili kuzuia kuzaana kwa umbu hao kupitia kwa maji yanayopatikana kwa vidibwi,” aliongezea King’oina.
Mhudumu huyo alisema kuwa wakazi wengi hupuuza masharti kama hayo ambayo mwishowe husababisha janga kubwa kwa jamii.
“Naomba wakazi wote kuzingatia masharti wanayopewa na Wizara ya Afya ili kujikinga na maafa mbalimbali,” alisema King’oina.