Share news tips with us here at Hivisasa

Msomi wa masuala ya ubaharia amesema sharti watu wajiepushe na kuenda kuogelea kwenye Bahari Hindi hasa wakati huu wa mvua ya El Nino, ambapo viwango vya maji huongezeka.

Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Mtongwe katika hafla ya kuwapa ushauri vijana pamoja na wakazi jinsi ya kujiepusha na kulemewa na mawimbi ya maji, wanapojipata katika hali ya dharura, Idris Juma, ambaye pia ni mwanajeshi wa zamani wa jeshi la wanamaji nchini, alisema kuwa mvua ya masika imeanza na wazazi sharti wawakanye wanao kuenda baharini kuogelea huko.

“Mvua nyingi huja na viwango na vipimo vya juu vya maji ambayo husababisha maji kuwa mengi baharini na hata kusababisha mawimbi kurudufika. Kwa namna hiyo, hakuhitajiki mtu yeyote kukaribia maji hayo kwani huwa rahisi kuwasomba watu wanaogelea, hasa iwapo hawana ujuzi wa kujikwamua kutoka kwenye maji mengi,” alisema Juma.

Aliongeza: “Watu wengi hapa huwa na ujuzi wa kadiri wakupiga mbizi lakini mawimbi yanapokuwa mazito baharini, ni muhali yeyote hata yule ambaye ana ujuzi kutumia motiboti, au mashua ili kukabili mawimbi. Ningependa kuwashauri wakazi kwa jumla kujiepusha na kuogelea bahari nyakati hizi,” alisema Juma.