Wakazi wa Lela iliyoko Kaunti ya Kisumu wameonywa dhidi ya kukata miti kiholela bila kuzingatia upanzi wa miche.
Wakionywa na naibu wa chifu wa eneo hilo, Lucas Ogada kwenye mkutano wa baraza la chifu ulioandaliwa mnamo siku ya Jumapili katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Lela, wakazi hao walitakiwa kupanda miche kadhaa kabla ya kukata mti mmoja.
''Iwapo unataka kukata mti, ni sharti kuhakikisha kwamba umepanda miche kadhaa ili kuendelea kuboresha makazi na mazingira ya misitu,'' alisema naibu chifu huyo.
Katika siku za hivi majuzi, wakazi katika eneo hilo waliingilia biashara ya uuzaji wa kuni, mbao na mkaa, hali ambayo imechangia ukataji wa miti kiholela.
Wengi katika eneo hilo wanategemea kuchoma mkaa ili kupata riziki huku wengine wakitumia wakati huo kibiashara. Unapotembea katika eneo hilo, utashuhudia shughuli za upasuaji mbao zikendeshwa vijijini huku macho yakikupa picha za mirundiko ya kuni zilizowekwa tayari kwa mauzo.
Hili linajiri wakati serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Mazingira inapohimiza wananchi kupanda miti kwa wingi.