Wakazi kutoka kaunti ya Mombasa wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuinua utalii kwa kuanza kuwa watalii wenyewe kama wenyeji.
Kulingana na mkuu wa Idara ya utalii katika Kaunti ya Mombasa Joab Tumbo, hatua hiyo itawezesha nchi kuimarisha viwango vya uchumi na pia itakuwa rahisi kuwashawishi watu wa asili ya kiafrika kuzuru mbuga tofauti.
Tumbo alisema kuwa ni wakati wa wakenya na waafrika kwa jumla kuanza kuinua uchumi wa nchi kwa namna mbali mbali utalii ukiwemo.
“Japokuwa watalii wanaoingia katika Kaunti ya Mombasa na eneo zima la pwani idadi yao bado ni ndogo, nina matumaini kuwa hivi karibuni idadi hiyo itaongezeka ikizingatiwa kuwa sasa nchi ya Kenya imeongeza juhudi zake katika vita dhidi ya ugaidi,” alisema Tumbo.
Alisema kuwa magaidi hao walisababisha nchi nyingi za ulaya kuwashauri raia wao kutozuru nchini kwa sababu ya kuhofia mashambulizi kutoka kwa makundi ya kiharamia ya Al Shabaab pamoja na kundi la Al Qaida.
Tumbo aliwashauri wakazi kuendelea kukumbatia mila na vile vile wawe wa kwanza kushawishi wengine kutoka nje ya pwani au nje ya nchi kwa kuonyesha utamaduni wa kipwani, huku akisisitiza umuhimu wa waafrika kutangaza utalii katika mataifa mengine kupitia mila na utamaduni.