Naibu wa chifu katika lokesheni ndogo ya Nyapedho, Douglas Okonji amewataka wakazi katika kijiji cha Anyiko kilichoko Tarafa ya Kopere kwenye Kaunti ndogo ya Muhoroni kufunika mashimo ya choo na visima wakati vikichimbwa.
Naibu wa chifu Okonji aliwataka wakazi katika eneo hilo kufunika mashimo yaliyochimbwa na yale ambayo hayajamalizika kuchimbwa ili kuepuka na mikasa inayoweza kutokea ya watu kutumbukia.
''Kama ni choo kichimbwe kwa siku chache na kujengwa, vile vile visima vya maji. Kuna hatari nyingi zinazoweza kutokea wakati mashimo hayo yanapokaa muda mrefu bila kufunikwa baada ya kuchimbwa,'' alisema naibu chifu Okonji.
Okonji alisema haya siku ya Jumanne wakati wa mazishi ya mtoto wa miaka miwili aliyefariki baada ya kutumbukia kwenye shimo lililonuiwa kujengwa choo.
Mtoto huyo alipatikana akiwa amefariki ndani ya shimo hilo baada ya kutoweka nyumbani siku tatu mbeleni. Mamake mtoto huyo aliwaambia waombolezaji kuwa, alimuacha mwanawe nyumbani akienda sokoni kununua chakula na aliporejea muda mfupi baadaye hakuweza kumuona mwanawe.
Mama aliambia huyo aliongezea kuwa hakudhania kama mwanawe angelikua ametumbukia kwenye shimo hilo na badala yake alimtafuta kwingineko, hadi pale mtu mmoja alipoenda kufunga ng'ombe katika eneo hilo na kufumbua kitendawili hicho kilichokuwa kimewakosesha usingizi familia yake kwa siku kadhaa.