Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima wa kaunti ya Nyamira wameombwa kuchukulia makini swala la utoshelezaji wa chakula kama njia mojawapo ya kupunguza visa vya ukosefu wa chakula kwenye kaunti hiyo. 

Akizungumza kwenye kijiji cha Mwongori, eneo la Borabu siku ya Jumapili, mshirikishi wa shirika la 'Hunger Free Group' nchini Erick Mbeche aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuekeza zaidi kwenye teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao ya shambani kama njia moja wapo ya kupambana na ukosefu wa chakula nchini. 

"Nawasihi wakazi wa eneo hili kukumbatia teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao mbalimbali ya shamba kama njia mojawapo ya kusaidia kupambana na ukosefu wa chakula nchini," alisema Mbeche. 

Afisa huyo aliongeza kwa kusema kuwa baadhi ya wakulima bado wanatumia mbinu za zamani kuhifadhi mazao ya shamba, hasa kwenye ghala, hali ambayo huweka mazao hayo kwenye hatari ya kushambuliwa na wadudu waharibifu. 

"Uhifadhi wa chakula ni swala ambalo bado lina utata huku Nyamira kwa kuwa wakulima wengi bado wanatumia mbinu za zamani za kuhifadhi mazao yao ya shamba, hali inayoweka mazao hayo kwenye hatari ya kushambuliwa na wadudu waharibifu," alisema Mbeche. 

Afisa huyoo aidha aliwaomba wakulima kuachana na tabia za kuwauzia madalali mazao yao kwa bei ya chini, na kuwashauri kuyauza mazao yao kwa bodi ya uhifadhi wa mazao nchini kwa bei nzuri. 

"Nawaomba wakulima kuacha tabia ya kuwauzia madalali mazao yao ya shamba kwa bei ya chini, badala ya kufanya hivyo, nawashauri wakulima hao kuuza mazao yao kwa bodi ya kitaifa ya uhifadhi mazao kwa bei nzuri," alishauri Mbeche. 

Akizungumzia swala lakufanyika mikutano ya kuwahamasisha wakulima kuhusiana na umuhimu wa kukumbatia kilimo, Mbeche alisema kuwa shirika lake lina mipango ya kufanya mikutano sawia na hiyo kote Nyamira ili kuhakikisha kuwa wakulima wa eneo hilo hawategemei chakula cha msaada. 

Haya yanajiri baada ya serikali ya kaunti ya Nyamira kuteuliwa kuongoza hafla yakusherehekea siku ya chakula duniani wiki moja iliyopita.