Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku idara ya taifa ya hali ya anga ikiwaonya watu dhidi ya mvua kubwa ya Elnino, Watu wanaoishi karibu na kingo za mito katika kaunti ya Kisii wameonywa dhidi ya kukaa maeneo yaliyo karibu na mito.

Akiongea siku ya Jumamosi mjini Kisii, mkurugenzi mkuu wa idara ya kilimo Nathan Soire amewataka wakulima wote na wakazi kwa jumla kujitahadharisha kulima hadi kwenye kingo za maji ya mito, akisema hali hiyo itasababisha mmonyoko wa udongo na kuwasihi kuanza kupanda miti karibu na kingo hizo za mito.

Ameonya kuwa iwapo wakazi hawatazingatia wito huo, huenda kukashuhudiwa maafa pamoja na mafuriko ya ajabu kwenye sehemu nyingi ikizingatiwa kuwa Kisii ni eneo la nyanda za juu na hupokea mvua kwa wingi nyakati kama hizi.

"Wakulima na wakazi wawe tayari kuondoka maeneo ambayo ni hatari, na nawaomba wale wakulima ambao wana mazoea ya kulima karibu na kingo za mito wakome kabisa, kufanya hivyo ni kusababisha kusombwa kwa udongo wenye rotuba," alionya afisaa huyo wa kilimo.

Hata hivyo, Soire aliahidi kuwa idara yao na ile ya maswala ya dharura kutoka kaunti ya Kisii watatoa ripoti mwafaka baada ya kuweka maafikiano yote siku ya Jumanne ili kuwapa wakazi wa kaunti mwelekeo mwafaka wa kufuata kuhusiana na tahadhari hiyo.