Mkurugenzi wa mazingira kwenye kaunti ya Nakuru ametoa onyo kali kwa wakazi wa mji wa Subukia ambao wamekuwa na mazoea ya kuchafua Mto Mumoi akisema chuma chao ki motoni.
Akizungumza na mwadishi huyu kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Ijumaa, Kiogora Muriithi alisema kwamba tayari amefika katika mto huo na kuona ulivyochafuliwa.
Alisema tayari ametoa onyo kali kwa baadhi ya wale aliowapata wakichafua mto huo, huku akisema kuwa walio karibu na mto huo wamekuwa wakitupa taka huku wengine wakiosha magari na pikipiki zao ndani ya mto huo.
“Wale walio katika mto huo na ambao wanaendelea kuweka taka kwenye mto wajue hilo jambo si nzuri kwa sababu wanaendelea kuchafua mazingira na huo mto unategemewa na watu wengi sana. Kwa hivyo, nimewaelezea wawache kufanya mambo yanayochafua mto huo kama kuosha magari na kuosha pikipiki na kutupa taka pale ndani. Wawache hayo maneno kwa sababu tutawashika na kuwachukulia hatua kali,” alisema Muriithi.
Mkurugenzi huyo aidha alisema kuwa kuna faini kwa muujibu wa sheria inayofaa kutozwa wanaochafua mazingira.
Alisema kuwa kutokana na hilo, amewataka wanaochafua mto huo na mito mingine kwenye kaunti ya Nakuru kujiepusha na hilo la sivyo wajipate pabaya.
Muriithi alionya kuwa atakayekamatwa kwa kosa la kuchafua mto huo na mito mingine katika kaunti ya Nakuru atahukumiwa kifungu cha zaidi ya miaka miwili gerezani au kutozwa faini ya nusu milioni kwenda juu.
Mkurugenzi huyo alisema idara ya mazingira kwenye kaunti imeanza msako wa kuwanasa wanaochafua mto huo na mito mingine katika kaunti ya Nakuru.
“Tumeanza msako wa kuweza kuhakikisha kuwa wale ambao wamekosa kutii sheria tunawashika na kuwashtaki. Faini si kidogo, ni elfu mia tano, milioni moja au miaka mbili au zaidi gerezani,” alisema Muriithi.
Mkurugenzi huyo ametoa onyo sawia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook.