Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi katika kaunti ndogo ya Kikuyu wameonywa dhidi ya kuwaajiri watoto waliochini ya miaka 18 kwa kuwa ni kinyume na sheria.

Haya yanajiri baada ya mwanamume mmoja pamoja na mkewe kutiwa mbaroni kwa kumwajiri msichana wa miaka 14 kama yaya katika nyumba yao katika eneo la Kikuyu.

Wawili hao walistakiwa na kundi la akina mama linalopiga kampeni dhidi ya dhuluma kwa wasichana katilka eneo la Kikuyu.

Akidhibitisha tukio hilo siku ya Ijumaa, ofisa mkuu wa kituo cha polisi cha Kikuyu, Inspekta Joshua Arende alisema kwamba visa vya aina hii vimezidi katika eneo la Kikuyu huku wanaoajiriwa wakisingizia umaskini.

Alieleza kwamba wazazi wa watoto hao wanachangia visa hivi kwa kuwaruhusu watoto wao kuajiriwa kisha kuwalisha wao wakiwa nyumbani.

"Ni hatia kubwa na wazazi wanaowatuma watoto wao kuajiriwa watahukumiwa kwa kukeuka sheria na haki za watoto," alisema Arende.

Alifafanua kwamba waajiri wanaowaajiri watoto hao, wanafanya hivyo kwa kuwa wanajua watoto hao hawana haki kisha kuwatumia vibaya na kuwalipa pesa kidogo.

Alisema kwamba ni hatia kwa yeyote kumwajiri mtoto aliye chini ya miaka 18 na atakayepatika atashtakiwa.

Arende alisema kwamba baadhi ya watoto huwacha shule kisha kutoroka nyumbani ili kupata ajira.

Alisema watoto wa aina hii wanafaa kurepotiwa pindi wanapoonekana wakiomba ajira popote pale.

Afisa huyo aliwahimiza waajiri kuhakikisha wanapokea stakabadhi kama vile kitambulisho ili kuhakikisha kwamba wanaajiri watu waliohitimu umri unaofaa.

Christine Kimani, mwenyekiti wa chama cha kutetea haki za watoto wa kike, alisema kwamba wawili hao walishtakiwa kwa kukiuka sheria na pia kuruhusu mtoto wa umri mdogo kuwa yaya katika nyumba yao.

Alieleza kuwa haki za watoto wa kike lazima zizingatiwe vilivyo ili kuhakikisha wasichana wanapata fursa ya kuenda shule.

Kimani alisema kwamba walikubaliana kama kundi, kumsomesha mtoto huyo ambaye mamake amekua akiugua kwa muda mrefu.

Msichana huyo pia ana ndugu wawili wadogo ambao wamekuwa wakiteseka baada ya kifo cha baba yao.

Alisema kwamba watawasomesha watatu hao na kuendelea na kampeni hiyo ya kutoajiri watoto.