Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi pamoja na wafanyabiashara walioko karibu na barabara kuu ya kutoka Likoni kuelekea Ukunda wameyataka mamlaka ya kusimamia utunzaji na ukarabati wa barabara kuweka matuta katika barabara hiyo ili kupunguza ajali ambazo zimekua za kila mara. 

Wakiongozwa na katibu wa wafanyabiashara katika eneo la Likoni Rashid Mwinyi, wafanyabiashara hao walisema kuwa katika siku za hivi karibuni, kumeshuhudiwa magari katika barabara hiyo pamoja wenye bodaboda wakigongana na kugonga hata watu ambao wanavuka barabara hiyo.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, walisema kuwa madereva wamekuwa na mtindo wa kuendesha magari kwa kasi bila kuzingatia sheria za trafiki na kuitaka idara hiyo kukaza misuli na kuwanasa madereva wanaovunja sheria.

Kiongozi huyo alitoa mfano wa ajali iliyotokea wiki jana Ijumaa ambayo ilihusisha pikipiki na gari la binafsi ambapo inasemekana wawili hao japokuwa walitoka na majeraha kidogo, walikuwa wanayaendesha magari yao kwa kasi, na katika mchakato wa kukwepa kumgonga mwenye pikipiki, gari hilo liliteleza na kugonga ukuta wa nyumba iliyokuwa kando ya barabara.

Wametaka serikali kuweka matuta kwa kila mita 50 ili madereva waweze kuwajibikia kazi yao na kuzingatia sheria za barabarani vilivyo.