Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa maeneo ya Ganjoni na Kizingo wamelalamikia kudorora kwa usalama katika barabara za Nyerere, Moi na baadhi ya barabara za kuunganisha mitaa hiyo.

Wakazi hao walilalamikia kushambuliwa na vijana wa mtaa hasa nyakati za usiku kwa kunyang'anywa hela wanapoenda na wanapotoka kwenye sala za jioni na asubuhi.

Akiongea siku ya Alhamisi, Hassan Faruq, ambaye ni mkazi wa Kizingo alisema kuwa vijana hao ambao hujumuisha watoto wanaorandaranda mitaani pamoja na baadhi ya vijana wengine ambao wanadaiwa kutoka mitaa ya mbali wamekuwa wakilenga nyakati zile watu huenda kuswali.

“Wahalifu hutegea sana sana vikundi vya watu ambao wako wachache kwa idadi ya wawili hadi sita, na kuwavamia kwa kutumia panga. Wengine hutumia choo cha binadamu ndio ukikosa kuwapa hela, wanakuchafua na hata kukupiga,” alisema Faruq.

Charles Lombe, ambaye ni mshirikishi wa usalama wa wakazi katika eneo la Reli katika mtaa wa Ganjoni, alidai kuwa swala la usalama limeanza kudorora tangu msako wa watumiaji wa dawa za kulevya kuanzishwa.

Lombe alidai kuwa baadhi ya wale ambao walikuwa kwenye biashara ya kuuza dawa hizo wamerudi mitaani kuibia watu.

Lombe aliitaka idara ya polisi kuanza kufanya uchunguzi na kupiga doria kila mara katika barabara kuu za mji huo ili kuwafurusha wakora hao.