Wakazi wa Kangundo katika Kaunti ya Machakos wameshauriwa kujiepusha na unywaji wa pombe ili kuepuka magonjwa kama ukimwi yanayoambukizwa mtu akiwa mlevi kwa kujihusisha katika ngono bila kinga.
Akiwahutubia wakazi katika baraza siku ya Jumanne, Naibu Kamishna wa Kangundo Bwana Samuel Njora aliwaeleza kuwa unywaji wa pombe humgeuza mtu mawazo na kumfanya afanye mambo atakayojuta baadaye.
Vilevile, alisema kuwa ulevi huathiri uwezo wa kufanya maamuzi na pia huvunja ndoa nyingi.
"Ulevi hauna faida yeyote kwani watu waambukizwa magonjwa hatari, ndoa zavunjika na watu wapoteza kazi zao, yote kwa ajili ya ulevi. Ni vyema mjiepushe na unywaji wa pombe,” alisema Njora.
Wakazi hao pia waliombwa kuripoti vilabu vinavyofunguliwa kabla ya wakati unaostahili ili wenyewe wachukuliwe hatua ya kisheria.
Bwana Njora pia aliwapa machifu wa eneo hilo ruhusa ya kukata miti ya mikaratusi iliyopandwa kando ya mito ili kuzuia mito kukauka mapema.
"Mito yakauka mapema kutokana na miti ya mikaratusi inayovuta maji kutoka mtoni. Machifu wana ruhusa ya kukata miti ya aina hiyo ili kuzuia kiangazi,” alisema Njora.