Huenda tatizo la mara kwa mara la uhaba wa maji kwa wakazi wa Kipkabus katika Kaunti ya Uasin Gishu likakabiliwa hivi karibuni.
Hii ni baada ya Kaunti ya Uasin Gishu kuzindua mradi wa maji wa kima cha Sh39m katika eneo hilo.
Mradi huo unalenga kusambaza maji kwa wakazi zaidi ya 5,000 kwenye mpaka kati ya kaunti hiyo na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet.
Maeneo ambayo yatanufaika pakubwa ni Kipkabus, Waunifor, Olare na maeneo mengine jirani.
Hapo awali, wenyeji wa maeneo hayo waliandamana kupinga ujenzi wa mabomba ya kusambaza maji katika eneo hilo kutoka katika Bwawa la Cheboen ambalo ni chanzo kikuu cha maji katika eneo hilo.
Wakiongozwa na Bw Joseph Chebore, wakazi hao walisema tangu ujenzi wa bomba la maji kutoka bwawa la Cheboen uanze, wananchi wa eneo hilo wamelazimika kutumia maji machafu ambayo yanatiririka kutoka katika mabomba yanayounganishwa.
Akizungumza ofisini mwake siku ya Jumanne, Mkuu wa Idara ya Maji na Mazingira katika Kaunti ya Uasin Gishu Bi Mary Njogu aliwataka wananchi hao kuwa na subira wakati mradi huo unapoendelea.
“Viongozi kutoka maeneo hayo walikutana kabla ya mradi huo kuanza ambapo walielewana kustahimili changamoto hii kwa muda ambapo mradi huu utakapokamilika,” alisema Njogu.
Bi Njogu alisema utawala wa Kaunti ya Uasin Gishu ukishirikiana na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet unatumia kila mbinu kuhakikishia kuwa wananchi wa kaunti hizo wanapata maji safi ya kukithi shughuli zao za kila siku.