Wakazi wa eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, wamehimizwa kuzingatia mpango wa Nyumba kumi na kuwatambua wahalifu ili watiwe nguvuni na maafisa wa usalama.
Kiongozi wa vijana katika eneo bunge la Kisauni, Maxwell Masai alisema kuwa asilimia kubwa ya vijana katika eneo hilo wamejiunga na makundi ya kihalifu na huvuruga usalama wa eneo hilo hali ambayo imewatia hofu wakazi wengi.
Akiongea katika eneo la Kiembeni huko Bamburi siku ya Jumatano, Masai alisema kwamba kupitia mpango wa Nyumba Kumi na wakazi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama, wakazi katika eneo hilo wataishi bila hofu yoyote, huku akiwahimiza mabalozi wa Nyuma Kumi kuwatambua vyema wakazi wao.
Alisema kwamba visa vya uhalifu katika kaunti ya Mombasa vimechangiwa na vijana kutojihusisha na maswala mbalimbali ya kimaendeleo.
Kiongozi huyo alisema kwamba kupitia kwa makundi ya kimaendeleo, vijana wengi watafaidika na miradi inayotolewa na serikali kuu na zile za kaunti.
"Tumekusanyika hapa kujadiliana maswala mbalimbali ya kuimarisha usalama ikiwemo kuwahimiza wakazi kuzingatia mpango wa Nyumba Kumi ili kuona kwamba kila balozi wa mpango huo anatambua wakazi wake. Hatua hiyo itasaidia pakubwa kupunguza visa vya uhalifu katika eneo letu,” alisema Masai.
Kiongozi huyo wa vijana amewahimiza wakazi kuzidi kuungana katika maswala ya kiusalama ili kuona kwamba mpango wa Nyumba Kumi katika eneo bunge zima la Kisauni unafaula na usalama wa wakazi unaimarishwa.