Wakenya wamehimizwa kuchukua hatua dhidi ya viongozi wafisadi ili kupunguza visa vya uporaji wa mali ya umma.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru, afisa wa mipango katika shirika linaloshughulikia maswala ya demokrasia kwenye Kaunti ya Nakuru 'Centre for Enhancing Democracy and Good Governance' (CEDGG) Masese Kemunche, alisema kuwa wananchi wanafaa kuchukuwa jukumu la kuwashtaki viongozi wafisadi.
“Shirika la CEDGG kwa wakati huu lingependa kuwahimiza Wakenya kukaa chonjo. Mnastahili kuchukua hatua ya kutaka wanaohusika kwenye wizi wa mali ya umma kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kemunche.
Aliongeza, “Tunaweza kuelekea mahakamani kama shirika lakini ni kutokana tu na juhudi za Wakenya kutaka kukabiliana na ufisadi ambapo mambo yatabadilika.”
Kemunche ametaka Wakenya kulichukulia swala la wizi wa mali ya umma kwa uzito.
Alisema kuwa katika siku za hivi maajuzi, matukio yanayoangaziwa na vyombo vya habari yanayoonyesha wizi wa mali ya uma kwenye serikali ya kitaifa na zile za kaunti yamekuwa yakichukuliwa kama mzaha.
‘Ilipobainika kuwa seikali ya kaunti ya Bungoma ilinunua toroli kumi zenye thamani ya shilingi milioni moja tukio hilo lilijaa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakicheka. Ripoti zilipotuarifu kuwa serikali ya Kaunti ya Meru ilinunua pazia za hospitali zenye thamani ya Sh7.8m, Wakenya walicheka tu huku wakiweka tukio hilo kwnye mitandao ya kijamii. Huo ulikuwa wakati mwafaka wa kuchukua hatua dhidi ya wale waliohusika,” alisema Kemunche.
Wakati huo huo, Kemunche amewataka wananchi kuweka kando suala la ukabila na kuchukua wajibu ili kukabiliana na janga la ufisadi.
Pamoja na hayo, amewahimiza wananchi kuungana pamoja kupinga ufisadi kwa kauli moja na pia kuitisha uwajibikaji kutoka kwa viongozi.
“Imebainika kuwa Wakenya kutokana na ukabila, wanadhani watu wa jamii yao wanapoiba, jamii nzima itanufaika. Dhana hii itazidi kuwa donda ndugu. Kama CEDGG tutazidi kufanya kila tuwezalo kama shirika kuhamasisha umma kuhusu jukumu lao la katika vita dhidi ya ufisadi,” alisema Kemunche.