Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakongwe na wanaoishi na ulemavu kutoka lokesheni ya Mwamonari eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini wamelalamikia kucheleweshwa kwa pesa zao.

Hii ni baada ya wakongwe hao kukita kambi katika ofisi ya chifu wa eneo hilo lililoko eneo la Sombogo ili kukabidhiwa pesa zao.

Wakizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Sombogo, wakongwe hao wakiongozwa na kiongozi wao Jackson Monari walisema kuwa huwa wanapata pesa zao baada ya miezi miwili kukamilika lakini wakati huu zimechelewa kupita kiasi.

Waliiomba serikali kuwakabidhi pesa hizo ili wajikimu kimaisha huku wakisema kuwa wanategemea pesa hizo.

“Tulikuja hapa mapema ili tukabidhiwe pesa zetu lakini tumefika na kupata hakuna pesa. Tufanye nini maana wengi tunazitegemea pesa hizi kwa kuwa ndizo zinatulisha,” alisema Monari.

“Tunaomba serikali ituletee pesa hizo kwa wakati ufaao maana kama mimi sina pa kutoa pesa kabisa na ninalala njaa kwani kwa kawaida huwa tunakabidhiwa pesa hizo baada ya miezi miwili. Pesa hizo zimechelewa wakati huu na tumeshindwa kubaini kiini cha jambo hili,” alisema Clemesiah Nyabonyi, mkongwe.

Wakongwe hao waliomba serikali kuweka mikakati ya kuwatumia pesa hizo kupitia huduma ya M-Pesa ili kuwarahisishia kazi hasa wale wanaotembea kutoka mbali.

“Mimi nimepanda pikipiki kutoka kwangu mpaka hapa na nimepata hakuna pesa. Sina nauli ya kurudi nyumbani. Itakuwa vizuri na rahisi kwetu ikiwa serikali itatutumia pesa kupitia huduma ya M-pesa ili wale tunaotoka mbali tufaidike,” alisema Shadrack Nyagesiba, anayeishi na ulemavu.