Shirikisho moja linalowaleta wakulima wa matunda na mboga katika Kaunti ya Kisii limewataka wakulima kujiandikisha kuepusha dhuluma kutoka kwa mawakala wanapowauzia bidhaa zao.
Kama njia mojawapo ya kuhakikisha wakulima kutoka Kaunti ya Kisii wanafaidi kutokana na mazao ya shambani, shirikisho limewataka wakulima hao kuwa tayari kujiandikisha katika jumuia hiyo ili kuwazuia mawakala ambao wamekuwa wakiwadhulumu kwa kuwalipa hela kidogo wanaponunua bidhaa zao.
Akizungumza siku ya Jumanne na Mwandishi huyu katika mji wa Kisii, mwenyekiti wa shirikisho hilo linalofahamika kama Embande Produce & Marketing Organisation Bw David Nyachae Abuya alisema shirika hilo linawalenga wakulima wa matabaka yote kuanzia mkulima wa chini hadi mkulima aliyekomaa katika masuala ya kilimo.
Shirika hilo ambalo hujihusisha na ukusanyaji wa matunda mbalimbali kama vile parachichi, matoke, nyanya na mengineyo, litahakikisha kila mmoja siye tu yule mkulima aliyejiandikisha bali wote wanao ari na moyo wa kushirikiana nao.
Abuya aliwataka mawakala ambao wamekuwa wakiwalaghai wakulima kwa muda mrefu kuwa tayari kwa kupata bidhaa kutoka Kaunti ya Kisii kutoka kwa jumuia yao, huku akisema kuwa wakulima sharti wajue haki yao.
Vile vile, mwenyekiti huyo alidokeza kuwa tayari mswada upo katika bunge la Kaunti ya Kisii ambao anadhamiria kuwapa nguvu za kutekeleza majukumu yao. Pia aliongeza kuwa mswada huo umebakisha awamu mbili tu ili kupitisha kuwa sheria katika kaunti hiyo.
Nyachae aliwashauri wakazi wote kutoka Kisii na Nyamira kuunga mkono azimio la jumuia hiyo ya wakulima na kusisitiza umuhimu wa wakulima pamoja na wafugaji kujiunga katika vikundi kama njia mojawapo ya kuwa na usemi mmoja wa mauzo na ununuzi wa bidhaa zao.