Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mkurugenzi mkuu wa kilimo katika Kaunti ya Kisii John Ndege akiongea katika maonyesho ya kilimo mjini Kisii siku ya Jumamosi aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuanza kufuga mbuzi.

Kufuatia maonyesho ya kilimo na biashara mjini Kisii, imebainika wazi kuwa ufugaji wa mbuzi miongoni mwa jamii ya Wakisii umedidimia kwa kiwango kikubwa mno, hali ambayo mkurugenzi Ndege amesema sharti ishughulikiwe.

Akiongea siku ya Ijumaa katika maonyesho hayo alipokuwa akimuonyesha Gavana James Ongwae aina mbali mbali ya mifugo ambayo idara hiyo ilileta, mkurugenzi Ndege aliwataka wakulima pamoja na wakazi ambao walihudhuria maonyesho hayo kuanza kukumbatia ufugaji wa mbuzi ili kujinufaisha kutokana na bidhaa zake kiuchumi na tiba pia.

Ndege alitaja umuhimu wa mbuzi kuwa mkubwa hasa maziwa yake akisema ni bora na yenye afya zaidi kuliko yale ya ng'ombe huku akisema kuwa maziwa hayo hutumika kama dawa ambapo husaidi kutibu maradhi ya kifua pia huimarisha kinga ya mwili na kuepusha mtu kulemewa na magonjwa.

Mkurugenzi huyo aliwataka wakazi kushauriana na maafisa wa kilimo na ufugaji katika idara ya kilimo Kisii ili kupata ujuzi maridhawa jinsi ya kufuga mbuzi na pia aliwataka wote waliohudhuria maonyesho hayo kumakinika ili wakirudi nyumbani waende kuwafunza wenzao baadhi ya ujuzi waliopata.

Asema kuwa ni rahisi kufuga mbuzi akiongeza kuwa mbuzi hutumia chakula kidogo ikilinganishwa na chakula cha ng'ombe, hali ambayo humweka katika nafasi bora zaidi mbele ya mifugo wengine.

"Tufuge mbuzi kwa vile ni rahisi kumtunza na haitaji sehemu kubwa kama ng'ombe na maziwa yake ni mazito na yenye afya zaidi,"

alisema mkurugenzi huyo wa kilimo.

kwineko akiongea katika maonyesho hayo ya kilimo na biashara, Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae aliwapongeza waandalizi wa hafla hizo huku akisema kuwa ataweka mikakati mahususi kuona maonyesho hayo yanakuwa na ushawishi mkubwa hadi katika nchi za ughaibuni kama njia mojawapo ya kuleta utalii katika kaunti hiyo.