Wakulima katika Kaunti ya Kisii wameonywa dhidi ya matapeli ambao wanaendelea kuuza mbolea ambayo haijaidhinishwa na Wizara ya Kilimo nchini.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika ofisi yake, Mkurugenzi mkuu wa Idara ya Kilimo katika Kaunti ya Kisii, Nathan Soire, alisema kuwa kumetokea watu ambao wamekuwa wakiuza mbolea ambayo haina kibali kutoka kwenye idara husika.
Soire alisema mbolea kama hiyo huwa na madhara kwenye mimea kwa sababu huwa imefunguliwa na hupoteza madini muhimu ya kurutubisha udongo na udhoofisha ustawi wa mimea.
Aidha, mkurugenzi huyo alisema kuwa kuna watu ambao wamekuwa wakinunua mbolea kutoka kwenye maghala ya serikali kwa kizingizio kuwa wanawakilisha wakulima kutoka maeneo fulani, na hao ndio washukiwa wakuu wa uuzaji wa mbolea hiyo.
Soire alisema kuwa mbolea hiyo ilikuwa ya serikali na huwa inapatiwa wakulima kwa bei ambayo imepunguzwa ili wale wakulima ambao hawana uwezo wa kununua mbolea kutoka maduka ya wafanyibiashara, waweze kunufaika.
”Yeyote ambaye atapatikana akijihusisha na biashara hiyo haramu hatua kali ya kisheria itachukuliwa dhidi yake,” alisema Soire.
Aliwataka wakulima kutoka kaunti ya Kisii ambao bado hawajapata mbolea hiyo kuenda katika ofisi ya chifu pamoja na ofisi ya kilimo katika eneo lake na kupata barua itakayotumiwa kama kibali cha kupokezwa mbolea hiyo ambayo uuzwa kwa Sh2,000 kinyume na ile ya maduka ambayo uuzwa kati ya Sh3,800 na Sh4,000.
Onyo hiyo limetolewa siku chache baada ya baadhi ya wakazi kutoka mitaa ya Kisii kama vile suneka na Daraja Mbili kutoa habari kuwa kuna baadhi ya wafanyibiashara ambao wameonekana wakiuza mbolea ya serikali.