Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima katika eneo la Nyanza wameomba serikali kuwasambazia mbolea ya upanzi mapema kabla ya muda kuyoyoma.

Kwa sasa matayarisho ya msimu mfupi yameanza kwenye maeneo mengi ya chemichemi. Wakulima eneo la Koru, Kaunti Ndogo ya Muhoroni wameiomba Wizara ya Kilimo katika eneo hilo kufanya mipango ya mapema ili kuwahami na bidhaa hiyo ambayo huwa adimu muda unapoyoyoma.

Katika maeneo ya chemichemi, wakulima wengi wameanza kutayarisha mashamba yao ili kuepuka mimea yao kuharibiwa na mafuriko ya maji kwenye maeneo hayo wakati mimea ikiwa ingali chini hali inayosababishwa na mvua nyingi ya msimu.

Hii ni baada ya wakulima wengi katika eneo hili kupata mavuno duni msimu uliopita kutokana na mashamba yao kujaa maji na kusomba mimea ilipokuwa ingali chini.

''Tumetaka kujiandaa mapema kwenye msimu huu mfupi ili kuepuka uharibifu mwingi katika mashamba ya chemichemi,'' alisema Musa Aroko aliyeongea na Mwandishi huyu mapema Alhamisi.

Aidha, mkulima huyo alisema kuwa amemaliza kuandaa shamba lake pamoja na mbegu na yupo tayari kwa upanzi wakati anaposubiri kuletewa mbolea.

Katika eneo la Miwani, shughuli ya kuandaa mashamba inaendelea huku mazao yanaendelea pia kutolewa mashambani.