Huku mvua ya El Nino ikitarajiwa kuanza mwezi wa Octoba, Kaunti ya Uasin Gishu inapanga zoezi la kuchanja mifugo katika kauti hio ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa ‘Rift Valley fever’ (RVF).
Akizungumza siku ya Ijumaa kwenye hafla ya kilimo biashara katika Chuo Kikuu cha Eldoret, mkuu wa Idara ya Kilimo katika Kaunti ya Uasin Gishu Cyril Cheruiyot, alisema kuwa maradhi hayo husababishwa na mvua kubwa.
Cheruiyot alisema ili kudhibiti hatari ya maambukizi hayo, kaunti ya Uasin Gishu kupitia Idara ya Kilimo, imeweka mikakati kabambe ya kuepuka maradhi hayo kama kuchanja mifugo kuanzia wiki ijayo.
"Naomba wakulima kutoka Kaunti ya Uasin Gishi kuleta mifugo wao ili wawezwe kuchanjwa dhidi ya maradhi hayo ambayo ni hatari kwa mifugo na yaweza kuwaua mifugo wengi kwa pamoja. Shughuli ya kuchanja itaanza saa mbili asubuhi siku ya Jumatatu," alisema Cheruiyot.
Aidha, mkuu huyo wa Idara ya Kilimo aliwashauri wakulima kushiriki katika ukulima wa aina mbali mbali ili kukabiliana na ushindani mkali unaoshuhudiwa katika soko la Afrika Mashariki.