Wakulima wa mahindi katika baadhi ya maeneo ya kanda ya Nyando, Kaunti ya Kisumu wanatarajia mavuno duni kutokana na kiangazi kilichotokea majuzi.
Mashamba ya mahindi katika maeneo ya Kuoyo Kodero, Kobura, Ka-Kango na kando kando mwa mto Ahero yameshuhudiwa kukauka kabla ya kukomaa, baada ya mvua kukatika siku chache zilizopita.
Eneo hilo lilishuhudia mvua nyingi wakati wa msimu wa upanzi, hali ambayo ilisababisha maji kufurika katika mashamba. Hali hiyo ya anga ilisababisha mahindi kujikokota kukua, hali ambayo imechangia ukaukaji wa haraka wa mahindi hayo wakati huu mfupi ambao kiangazi kimeshuhudiwa.
Monica Adikinyi ni mmoja wa wakulima wa viwango vya juu ambaye msimu huu anatarajia mavuno machache kutoka kwenye shamba lake la ekari tatu.
''Mavuno ya msimu huu yatakuwa machache kulingana na dalili ambazo tumeanza kushuhudia kwa sasa. Mahindi yalichukua muda mrefu katika mashamba hali ambayo ilisababishwa na hali mbaya ya anga,'' amesema Adikinyi.
Akiongea na Waandishi wa habari waliomtembelea nyumbani mwake mapema Jumamosi, mkulima huyo alisema imekuwa vigumu kwa wakulima katika maeneo hayo kutabiri wakati mwafaka wa upanzi, ikizingatiwa kuwa hali ya anga inaenda ikibadilika kila msimu.
Aidha, Adikinyi alisema kuwa pana haja ya wakulima wa eneo hilo kuanzishiwa ukulima wa unyunyizaji maji mimea, ili kuweza kufaidika na ukulima nyakazi zoke.