Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vikundi vya wakulima wa majani chai katika kaunti ya Nyamira vimeshauriwa kukopa pesa kutoka kwa benki ili kutunza mmea huo.

Wito huo umetolewa ili wakulima kuacha tabia ya kupanda mahindi pamoja na mmea huo, na kuchukua mkopo ili kutunza na kuulinda kwa njia ya uwazi ili waje kunufaika kwa siku za usoni.

Akizungumza na wakulima hao wa majani chai siku ya Jumanne katika kiwanda cha Nyankoba kilichoko katika kaunti ya Nyamira, mshauri mkuu wa benki ya dunia Charles Mochama aliwaomba wakulima wa majani chai kukopa kutoka kwa benki ya Equity na ile ya Family, ambapo benki ya dunia imeweka pesa zao ambazo wanaweza kukabidhiwa kama mikopo na kutozwa kiwango cha chini cha riba cha asilimia nane kwa pesa zile watakazokabidhiwa kwa kila mwaka.

“Benki ya dunia imeweka pesa zetu kwa benki ya Equity na ile Familily, yeyote yuko na nia ya kupata mikopo umekaribishwa na kiwango cha faida unatozwa kwa kila mwaka ni asilimia nane pekee, ambacho ni kiwango cha chini ikilinganishwa na mikopo mingine,” alisema Mochama.

“Naomba wale wakulima wa mmea wa majani chai kukopa pesa na kutunza mmea huo ili mje kujisaidia nyakati zijanzo,” aliongezea.

Aidha, mshauri huyo aliomba wakulima hao wa majani chai pia kuanzisha kilimo kingine ili wasipovuna vyema kwa majani chai wawe wana mahala pengine pa kuvuna.

“Naomba wakulima wa majani chai mtafute kilimo kingine  ambacho mtavuna mnapokosa kuvuna kwa majani chai ili eneo la Kisii liweze kuinuka kimaendeleo,” aliongezea.