Share news tips with us here at Hivisasa

Huku vita vya kupigana na utumizi na uuzaji wa dawa za kulevya kwa vijana katika eneo la pwani vikishika kasi, kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema kuwa walanguzi hao wameanza kubadili mbinu za kusambaza dawa hizo kwa wateja wao.

Marwa alisema kuwa wauzaji wa dawa hizo wamekuwa wakibadilisha majina yao, na hata kuwatishia wateja wao kuwa watawaua iwapo watatoa ripoti kwenye idara ya polisi kuhusiana na shughuli zao za kuuza dawa hizo.

Akiongea katika uga wa umma wa Mombasa siku ya Jumanne katika sherehe ya kuadhimisha siku ya Mashujaa, kamishna huyo alisema kuwa baadhi ya wasambaji mihadarati wameanza kujifanya kuwa walinda usalama wa kimaasai, ambapo aliitaka idara ya polisi kufanya uchunguzi na kubaini baadhi ya vijana ambao wanatoa usalama kwa kuvaa mavazi ya kimaasai.

“Walanguzi hawa kila mara wamekuwa wakibadili mbinu za kuuza dawa hizi kwa wateja wao. Baadhi ya walanguzi wanajifanya kuwa walinzi ambao huvaa nguo za kimaasai, na wengine hutumia majina tofauti mbali na yale yaliyo kwenye vitambulisho vyao. Tuko tayari kupigana na magenge hayo ya kuuza mihadarati,” alisema Marwa.

Marwa pia alisema kuwa kundi ambalo limekuwa likiwahangaisha wananchi la 'Mombasa Crime Alert' halitambuliki na serikali na kuwataka vijana hao kuwa tayari kupambana na mkono wa sheria.

Aidha, alisema kuwa bado wataendelea kushirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa kupiga vita uhalifu na kuweka juhudi za kuimarisha usalama ambao umedorora kwa siku za hivi karibuni.