Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa shirika la walemavu, ‘Association Of Physical Disabled of Kenya (APDK)’ amesema serikali ya kitaifa imejizatiti kuzingatia haki za walemavu kwa kuhakikisha kwamba mahitaji yao yanazingatiwa, lakini bado haijafanya ya kutosha.

Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Nakuru, Wilfred Owako, alisema sheria iliyopitishwa wakati Mwai Kibaki alikuwa rais, inafaa ifanyiwe marekebisho zaidi ya kuwafaa walemavu, licha ya kutenga fedha za kuwasaidia wenye changamoto za kimaumbile.

Owako alisema angalau kwa kiasi fulani fedha hizo zinawafikia walemavu mashinani, japo hazitoshi kwa sababu wengi wao wana kiu ya kupata elimu na maisha bora.

Alidokeza kwamba serikali ya kaunti ya Nakuru ilitenga Sh55m, ambazo zilikuwa zitolewe kwa kila wodi katika mwaka wa kifedha 2014/15, lakini pesa hizo zimekaa bila kutumiwa kwa sababu hakuna sheria iliyowekwa ya kuzigawa.

“Mwaka huu wa kifedha 2015/16, tungetaka watenge pesa zaidi ili tufaidike manake tuna changamoto za kifedha,” alisema Owako.

Aidha, aliitaka serikali ya kaunti ya Nakuru kuajiri watu wengi walemavu, kama njia moja ya kuwawezesha kiuchumi.

“Tunataka watu wengi katika kaunti wafunzwe namna ya kuwasiliana na walemavu kwa ishara na nyumba zinapojengwa wajenzi wazingatie haki za wanaotumia viti vya magurudumu, na pia vyoo na bafu za walemavu zijengwe,” alisema Owako.

Bii Moli Adero, anayefanya kazi kama daktari wa afya ya jamii, alisema kwamba walemavu na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanakabiliwa na changamoto nyingi.

“Jamii iache kudhalilisha watu walio na ulemavu na pia wanaoishi na virusi vya HIV, hakuna mtu huchagua kuwa mlemavu,” alisema Adero.