Walemavu wanaiomba serikali kuwatafutia njia mbadala ya kutumia ili kuepuka msongamano wa abiria na magari katika kivuko cha feri.
Akizungumza siku ya Jumatatu na mwanahabari huyu, mzee Karisa Babu, mwenye ulemavu, alisisitiza kuwa anapata wakati mgumu kuvuka katika kivuko hicho hasa wakati wa asubui na jioni ikizingatiwa ndio wakati kuna msongamano wa abiria na magari.
Babu aliongeza kuwa kidogo aangushwe majini wakati watu walipoanza kusukumana katika kisa kilichofanyika Jumatatu asbuhi.
“Kidogo nianguke majini baada ya kusukumwa na watu wenye nguvu, na hali hii yangu inakuwa vigumu kujitetea,” alisema Babu.
Aidha, aliomba usimamzi wa shirika la feri kuharakisha kutatua tatizo hilo kwa haraka ili hali irudi shwari.
Siku ya Jumtatu watu 15 walijeruhiwa baada ya msongamano mkubwa kushuhudiwa katika kivuko cha feri cha Likoni kutokana na upungufu wa feri zinazotoa huduma bandarini.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Pwani, miongoni mwao akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye sasa atalazimika kufanya mtihani wa kitaifa akiwa hospitalini.
Kwa upande wake, kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa ameiomba serikali ya kitaifa, kupitia kwa wizara ya uchukuzi nchini kumpiga kalamu mkurugenzi wa shirika hilo Hassan Musa, kwa madai ya kuzembea kazini.