Walimu wakuu wa shule za umma mjini Mombasa ambao shule zao hazijapata hati miliki wametakiwa waiandikie barau wizara ya ardhi nchini iwape stakabadhi hizo, ili kuzuia visa vya unyakuzi wa ardhi za shule.
Haya ni kutokana na kukithiri kwa visa vya unyakuzi wa ardhi na kufurushwa kwa wakazi katika baadhi ya maeneo mjini Mombasa kwa madai kuwa ardhi wanazoishi zinamilikiwa na watu flani kinyume na matarajio ya wakaazi hao.
Mwito huo umetolewa na mwanaharakati wa maswala ya kisiasa na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa Joseph Masai, ambaye alionya kuwa wale walionyakuwa ardhi za shule watachukuliwa hatua.
“Tungependa kuwaambia walimu wakuu wa shule za umma wawe makini na baadhi ya mabwenyenye wanalenga kunyakua ardhi za umma haswa ardhi za shule. Wakati umefika sasa walimu wote wakuu kujitokeza na kuiandikia barua ya kuomba haki miliki za shule ili kuepukana na migogoro ya unyakuzi wa ardhi za shule,” alisema Masai.
Masai aliongeza kwamba huenda miradi tofauti ya shule ikakosa kutekelezwa iwapo shule nyingi mjini humo zitakosa hati miliki za ardhi zao, hatua ambayo imekuwa tishio kwa wanyakuzi wa ardhi wanaonyemelea ardhi za umma na kuzinyakua.
Mapendekezo yake yamejiri baada ya shule nyingi za umma kubaini kutokuwa na hati miliki za ardhi, jambo ambalo limewatia wasiwasi wazazi wengi wa shule hizo mjini Mombasa.