Share news tips with us here at Hivisasa

Huku maandamano ya walimu yakiendelea kote nchini walimu katika kaunti ya Kisii siku ya Jumatatu waling’oa lango kuu la kuingia shule ya upili ya wavulana ya Kisii na kuharibu ua wa mbao unaozingira shule ya upili ya wasichana ya Kereri.

Kwenye maandamano hayo ambayo yalizua fujo baada ya maafisaa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Central kuanza kukabiliana na walimu hao pamoja na baadhi ya wananchi ambao waliwaunga mkono, ambapo waliingia hadi shule ya wavulana ya Kisii na ile ya wasichana ya Kereri na kuwataka baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa humo shuleni kuondoka.

Kulingana na katibu mkuu wa Knut katika wilaya ya Kisii ya kati Bwana Shem Nyaundi, walimu walichukua hatua hii ili kuionyesha serikali ya Jubilee kuwa hawarudi nyuma katika harakati za kupigania haki za walimu.

Aliwashauri wanafunzi kuenda nyumbani kusomea huko na kushauriana wao kwa wao kuhusiana na masuala ya masomo huku wanapoendelea kutarajia suala lao kuangaziwa na serikali.

Pia aliitaka serikali kutimiza ahadi ililzotoa kwao akimwomba Rais Uhuru Kenyatta kuasi mtindo wa serikali za hapo awali aliotaja kuwa wamekuwa wakiendeleaza mtindo wa kuwanyanyasa walimu.

“Serikali sharti ilipe walimu nyongeza yao vile mahakama iliamua na serikali ya Jubelee ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Wiliam Ruto, kama hatulipwi tutaendelea na mgomo hadi serikali itulipa hela,” alisema Bwana Nyaundi.