Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ya kuajiri walimu nchini TSC tawi la Mombasa imetishia kuwapa barua za adhamu walimu wanaoshiriki mgomo katika kaunti hiyo.

Akiongea mjini Mombasa na wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Mkurugenzi wa tume hiyo ya TSC tawi la Mombasa Ibrahim Rugut alisema kuwa maafisa wa tume hiyo wametumwa katika shule za msingi na upili kukusanya ripoti ya walimu ambao hawajarudi shuleni.

Kulingana na Rugut, walimu wa shule zaidi ya shule 100 za msingi na 35 za upili katika kaunti hiyo, watapewa barua za adhabu kutokana na kukosa kuendeleza masomo na kushiriki mgomo usio kuwa halali kulingana na tume hiyo.

“Maafisa wa tume hii wako nyanjani kukusanya ripoti kutoka kwa walimu wakuu wa shule. Wale waliyokosa kufika shuleni hata baada ya tume hiyo kutangaza kuwa mgomo wanaoshiriki sio halali basi watachukuliwa hatua za nidhamu,” alisema Rugut.

Rugut ameshikilia kuwa walimu wanafaa kurudi shuleni na kuendeleza masomo akisema kuwa swala lao litatatuliwa na tume hiyo, Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Fedha.

Aidha, amekashifu hatua ya Chama cha walimu nchini Knut na Kuppet, kwa kuanzisha mgomo bila kutoa notisi kwa tume hiyo akisema kuwa vyama hivyo vimekosa maadili na viongozi wa vyama hivyo wanafaa kuadhibiwa kwa kukosa kuzingatia sheria.

“Vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini vimekosa mwelekeo kwa kuwashinikiza walimu kushiriki mgomo bila ya kutoa notisi ya siku 14, na notisi nyingine ya siku saba. Wangesubiri kesi zilizoko mahakamani kukamilika ndio wakaitisha mgomo. Sasa walimu wanaoshiriki mgomo wataadhibiwa,” aliongezea Rugut.

Haya yamejiri huku viongozi wa chama cha walimu nchini Knut na Kuppet wakielekea mahakamani kupinga agizo la TSC kuwa mgomo walimu wanaoshiriki sio halali pamoja na kuishinikiza serikali kuwalipa nyongeza yao ya asilimia 50 na 60.