Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa chama cha Knut tawi la Gucha Kusini, Kaunti ya kisii, Joseph Makabe, ameiambia tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuwa hata wakifuta walimu hawatarudi darasani kamwe hadi waongezwe nyongeza yao ya mshahara.

Hii ni baada ya tume hiyo ya TSC kutishia kuwafuta kazi walimu ambao hawatarejea kazini kwa kukiuka ombi la mwajiri wao la kurudi kazini.

Akizungumza siku ya Alhamisi wakati alikuwa anaongoza maandamao katika eneo la Etago na Tabaka, eneo bunge la Mugirango Kusini, katibu huyo alisema hawatarudi kazini hadi waongezewe mshahara.

Wakati huo huo, katibu huyo aliomba Rais Uhuru Kenyatta kujali maslahi ya watoto na wazazi kwa kuwaongezea walimu nyongeza yao jinsi mahakama ilivyoagiza.

“Ni aibu kubwa sana watoto kuendelea kukaa nje wakati serikali inaendelea kuendesha shughuli za serikali humu nchini. Naomba Uhuru na Ruto kuhakikisha walimu wamelipwa ili kurudi darasani na kuwafundisha watoto,” alisema Makabe.

Aliongezea “Lile ambalo ningependa kuwasilisha kwa tume ya TSC ni kuwa hata wafute walimu 20,000 hatutaogopa na kurudi darasani. Hata wafute walimu wote 288,000 bado harutarudi darasani.”