Walimu katika shule zilizo karibu na maeneo ya soko katika Kaunti ya Kisumu wametakiwa kuwachunga wanafunzi na kuwazuia kutoka nje ya shule wakati usiotakikana.
Ombi hilo ni kupunguza visa vya wanafunzi kurandaranda sokoni wakati wa masomo. Wazazi kutoka tarafa ya Lela, Maseno walitoa hoja hiyo mnamo siku ya Ijumaa kwenye mkutano wa wazazi na walimu katika Shule ya Msingi ya Lela.
Wakihutubu, wazazi hao walidokeza kwamba baadhi ya wanafunzi kwenye shule nyingi za eneo hilo huonekana wakizurura katika soko za eneo hilo nyakati wenzao wamo darasani.
''Tumewashuhudia wengi wa wanafunzi kwenye sare za shule wakizunguka huku na kule sokoni, hali ambayo tunahofia huenda ikachangia utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi na kusababisha matokeo mabaya kwenye mitihani,'' alisema Philip Nyangweso, mmoja wa wazazi wakati wa mkutano huo.
Aidha, wazazi hao walitaka kujua kutoka kwa walimu iwapo nao pia wanalijua tatizo hilo ambalo limeonekana kusakama shule nyingi za eneo hilo zikiwemo za mabueni.
Pia walitaka shule hizo kuzingirwa kwa ua ili kudhibiti hali hiyo. Naibu wa mwalimu mkuu, Peter Odhiambo aliwaelezea wazazi hao kuwa kuna haja yao kushirikiana na walimu ili kudhibiti hali hiyyo, akisema kwamba hali hiyo huchangiwa na utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi kutokana na malezi mabaya ya baadhi ya wazazi.