Wanabiashara mjini Kisii wameiomba serikali ya kaunti kuwatafutia soko ya ndizi ili kujiimarisha kibiashara.
Wakizungumza na mwandishi huyu katika eneo la Market mjini Kisii wanapouzia ndizi zao, wanabiashara hao walilalamika kuwa hawana soko kwa zao lao.
“Mimi nilileta ndizi ambazo nilinunua siku ya Jumatatu wiki jana, na hadi sasa sijauza na hiyo ni hasara kwangu maana ningekuwa ningeleta nyingine na kila siku nasafiri na siuzi,” alihoji Elijah Ongwae, mwanabiashara.
“Tunaomba serikali ya kaunti itutafutie soko ili tuwe tunauza ndizi haraka, na kilichopelekea kutochukuliwa kwa ndizi ni vile ndizi zimekuwa nyingi katika mashamba ya eneo la Kisii,” alisema Wilfred Ong’era, mwabiashara mwingine.
Haya yanajiri baada ya gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Alex Tolgos kutembelea kaunti ya Kisii na kukiri kuwa kaunti ya Kisii ikishirikiana na kaunti hiyo biashara ya ndizi itaimarishwa kati ya kaunti hizo mbili, jambo ambalo wanabiashara husika wameomba serikali ya Kisii kutilia maanani.
“Ni busara serikali ya kaunti ya Kisii kuyafuata yale waliongea na gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet kwa kutafuta soko ya ndizi, tunaona serikali ya Kisii hakuchukulia maanani swala hilo na tunaendelea kukabiliana na hasara kutokana na ukosefu wa ununuzi,” aliongezea Wilfred Ong’era.
Kibarua sasa ni kwa serikali ya kaunti kusikia kilio cha wanabiashara na kuwatafutia soko wanabiashara hao ili biashara yao inawiri.