Wanafunzi waliofadhiliwa na serikali kuu pamoja na ile ya kaunti kwa ushirikiano na serikali ya Japan walifuzu siku ya Ijumaa kutoka chuo cha masomo ya ujenzi mjini Kisii.
Kama njia mojawapo ya kuboresha na kuimarisha ujenzi wa barabara, serikali iliwezesha wanafunzi wa kitengo cha uhandisi wa ujenzi wa barabara na ukarabati wa miundo msingi kufuzu, kwenye hafla iliyokuwa ya kufana.
Vijana hao zaidi ya mia nne, ambao waliwakilisha kaunti 42 kutoka kote nchini waliwekewa taji zao na tayari kuenda nje kuwakilisha nchi katika ujenzi wa barabara na ukarabati katika kaunti mbali mbali humu nchini.
Akiongea katika hafla hiyo, naibu balozi wa Japan Mikio Mori aliwataka wanafunzi hao kujitahidi ili kuifaa nchi ya Kenya pamoja na nchi zinazowakilisha Afrika mashariki kwa jumla.
Mori alisema kuwa serikali ya Japan itafanya kila liwezekanalo kuona kwamba nchi ya Kenya inafaidi kutoka miradi mbali mbali inayofadhiliwa na nchi hiyo, na aliwashukuru viongozi wa kaunti ya Kisii pamoja na Nyamira kwa kuwaalika kwenye taasisi hiyo.
Pia aliishukuru serikali kuu ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuonyesha moyo wa kuendeleza uhusiano ulioko kati yao na nchi hiyo.
Naibu balozi huyo aliongeza kusema kuwa baadhi ya wanafunzi ambao walifuzu watachukuliwa na shirika la CORE, ambalo ni mojayapo ya wafadhili wa mafunzo hayo ya vijana kwa ushirikiano na serikali ya Kenya.
Naye msimamizi mkuu wa taasisi hiyo John Ontomwa aliwataka vijana waliofuzu kuhakikisha kuwa wanajiunga na taasisi ya uhandisi wa barabara ili kunoa makali zaidi.