Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku Chuo kikuu cha ufundi cha Mombasa kikifungwa rasmi baada ya ghasia kuzushwa na wanafunzi wa chuo hicho, wito umetolewa kwa wanafunzi kutafuta njia mbadala za kupata suluhu tatizo linapotokea.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu muda mfupi tu baada ya wanafunzi wa chuo hicho cha Mombasa kuzua fujo wakilalamikia kuongezwa kwa karo, katibu wa jumuia ya wafanyibiashara katika mtaa wa Tudor, Nelson Muramba, alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekosa hekima hasa kunapozuka tatizo baina yao na mamlaka ya chuo husika.

Alisema kuwa mara nyingi wanafunzi hao hutolea hasira zao kwenye mali na biashara za watu.

Muramba aliwashtumu viongozi wa wanafunzi kwa utepetevu na kukosa kuwajibikia nafasi yao ya kuwaelekeza wanafunzi hao kwa njia nzuri bila hata kujihusisha kwenye maandamano.

Alisema kuwa hilo ni suala ambalo lilihitaji mdahalo kati ya usimamizi wa chuo na wawakilishi wa wanafunzi.

Katibu huyo alisema kuwa wanafunzi wanapaswa kufahamu kuwa kuna njia nyingine za kutafuta maafikiano.

"Sio lazima wanafunzi kujihusisha kwenye migomo wanapokumbwa na matatizo. Kuna mbinu zaidi ya tano zinazoweza kutumika kutafuta suluhu kabla ya kuhiari kuanza kuandamana na kuharibu mali ya wenyewe kinyume na sheria," alisema Muramba.

Kwenye ghasia hizo, mali nyingi na biashara ziliporwa na magari kuchomwa yakiwemo malori ya kuzoa taka ya serikali ya Kaunti ya Mombasa.